VIJANA MSIWE
KAMA NYAMA YA KWENYE JOKOFU ……………11/04/2019
“ Vijana legelege, wasiopenda kufanya kazi,
wanaotegemea kutunzwa na wazazi wao muda huo umekwisha, fanyeni kazi kwa bidii
ili muweze kutoka hapo mliposimama miaka yote”
Maneno hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki
la Mpanda na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu teule la Mbeya Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga katika
kongamano la vijana Jimboni Mpanda.
Kongamano hilo lililofanyika Parokia ya Kanisa Kuu
Mpanda katika ukumbi wa Mikutano kuanzia tarehe 10-14.4.2019 lilifunguliwa
rasmi na Mhashamu Baba Askofu sambamba na Mkurugenzi wa Vijana Jimbo Padre JohnBosco
Misigalo ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mamba liliwakutanisha vijana zaidi
ya 200 kutoka Parokia 14 kati 16 za Jimbo.
Wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo Mhashamu Baba
Askofu alikumbushia majukumu ya vijana katika kanisa ambapo amesema kuwa “
Uzima wa Kanisa ni Vijana”, vijana hai hulijenga kanisa kwa majitoleo
mbalimbali lakini kulijenga kanisa inategemeana na namna ambavyo vijana
mnashiriki katika shughuli kwa ushirikiano, umoja , unyenyekevu na mahusiano
mazuri. Haya yote hayawezi kufanikiwa ikiwa kijana atakuwa ametengeneza
mazingira mabovu ya kujitegemea kama “NYAMA YA JOKOFU”.
Nyaisonga amesema ulimwengu wa sasa umejawa na
vijana wengi wenye taaluma mbalimbali, wasomi, wajasiliamali na makundi
mengine, “Tumieni ujuzi mliopewa na mwenyezi Mungu kwa kufanya kazi kwa bidii,
kwa kufanya hivo mtazikomboa familia zenu na kanisa la Mungu. Amesema kama
mwaka uliopita ulikwama mahali basi angalia namna ya kupiga hatua ndefu zaidi
kufikia malengo, lakini katika yote mkumbuke kusali, kufanya toba ili maisha
yenu yawe yanayompendeza Mungu siku zote.
Aidha amewapongeza vijana wote kwa moyo wa
majitoleo kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo pasi na changamoto
zinawakabiri” nimefurahi sana kuwaona kwa wingi, sasa naamini Jimbo la Mpanda
lina hazina kubwa hapo baadae, muendelee kuwa na moyo huo na siku zote mpende
kushiriki kazi za kanisa kwani maisha ya hapa duniani ni ubatili Mtupu.
Mwisho : Mhashamu Baba askofu amewapongea kwa
namna ya pekee vijana wakatoliki kote nchini wanaotumia vipawa walivyojaliwa na
mwenyezi Mungu kufanya kazi za Kanisa bila kujali muda wanaopoteza na nguvu nyingi,
“ lakini katika yote niwatie moyo yeyote afanyaye kazi kwa bidii hupata ujira
wake, kwa kufanya kazi za kanisa mnajiwekea hazina isiyofutika mbinguni.
Nawatakia maandalizi mema ya Sikuku ya Pasaka ,
tukumbuke kufanya toba ili tufufuke pamoja na Yesu Mkombozi wa Miasha Yetu.
NA SUZAN KANENKA
MKURUGENZI WA HABARI
JIMBO KATOLIKI MPANDA
No comments:
Post a Comment