KAREMA, KANISA LA KIHISTORIA |
CHIMBUKO LA UKRISTO JIMBO KATOLIKI LA MPANDA
Ukristo
Jimbo Katoliki la Mpanda uliingia tangu mwaka 10.07.1885 kupitia Karema, lakini
hatuwezi kuzungumzia ukristo wa Jimbo la Mpanda bila kugusa majimbo ya
Sumbawanga na Mbeya. Hii inatokana na kuwa Karema ndio kitovu cha Ukristo kwa
Majimbo Haya.
Wamisionari
waafrika ( White Fathers) walitumwa katika Afrika Mashariki kwenye maziwa makuu
ambapo mwanzilishi wa shirika hilo Kadinari Lavigerie pamoja na uinjilishaji alilenga pia kupigania
uhuru wa watumwa. Katika harakati za kueneza dini nchini waliingia Bagamoyo
wakitokea Zanzibar mnamo mwaka 1868, baada ya Bagamoto walianza kutembea maeneo
mbalimbali yakiwemo maeneo ya mwambao wa ziwa Tanganyika, Tabora, Mwanza,
Kigoma (Ujiji) hadi Rumonge (Burundi).
Mwaka
1885 wamisionari waliingia Karema na hapa sasa ndo tutakapofahamu historia ya
ukatoliki Jimbo la Mpanda. Kama ilivo ada, baada ya wamisionari hawa kufika
Karema walikuwa na kazi kubwa ya kueneza injili , karema iliyo mwambao wa ziwa
Tanganyika na maeneo jirani ndiko wafanyabiashara ya utumwa walivuka
kutoka Kongo wakielekea katika soko la
watumwa. Haikuwa kazi rahisi kwao kutangaza na kueneza injili ipasavyo, pasi na
changamoto walijenga misioni (KANISA) ambalo liliwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni na mnamo
tarehe 15.08 Kanisa lilibarikiwa na kutumiwa kwa ajili ya sala, mafundisho na
maadhimisho ya misa takatifu.
Maaskofu
wa kwanza , Mapadre na Mabruda
walishirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha dini inaenea kwa watu wote. Na
kipindi hicho Misioni hiyo ilipewa hadi ya Vikarieti kwa Jina la Vikarieti ya
Tanganyika ambayo iliongozwa na Mh Baba Askofu wa Kwanza Jean Baptist Charbonnier aliliongoza kanisa
kuanzia mwaka 1885 ya ukristo kuingia Karema hadi mwaka 1888. Maaskofu wengine
wamisionari walioongoza ni pamoja na Leonce Bridox mwaka 1888 hadi 1890 na
Adolhe Lechaptois mwaka 1891 hadi 1919. Tunaweza kusema hao ni viongozi
waliopigania ukristo kwa hali na mali
kwa kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili na kwa namna ya pekee kuwakomboa
watumwa katika kipindi hicho cha mwanzo wa ukristo Karema. Karema iliendelea
kuwa na hadhi ya vikarieti ya Tanganyika hadi mwaka 1953 chini ya Mhashamu
Askofu James Siddle na ikapewa hadhi ya kuwa jimbo. Mwaka 1958 waamini wa Jimbo
la Karema walipata Askofu wa kwanza mzalendo na mzaliwa wa Karema Mhashamu Baba
Askofu Charles Msakila.
Wabende
ambao ni wenyeji wa Karema na maeneo jirani waliipata injili na kufuata
mafundisho ya dini japo kazi haikuwa rahisi kutokana na Tamaduni zao za
kikabila, ilikuwa vigumu zaidi kubadili kile ambacho wamerithishwa kutoka enzi
za mababu. Mfano wabende waliamini kuwa mwanaume hapaswi kuoa mwanamke mmoja
kwao wao kuwa na mwanamke mmoja ni dharau . imani hiyo ilikuwa changamoto kubwa
wamisionari kubadili mitazamo na ukizingatia kanisa Katoliki linafundisha juu
ya Ndoa ya Mke mmoja tu. Uwepo wa watemi pia ulichangia imani kuenea taratibu
kutokana na kuamini mila na desturi zao kuwa sahihi.
Baada
ya Injili kuhubiriwa , watu kubatizwa wamisionari walianzisha Shule za msingi
lengo likiwa ni kuwapatia Elimu ya Jamii waumini ili kukomboa fikra sambamba na
kuanzishwa kwa zahanati ambapo walipata hudumu ya Afya kwa ukaribu zaidi.
Kutokana
na malengo ya wamisionari wa Afrika kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili
ikiwemo kuwakomboa watumwa, nia ilikuwa kuwakomboa hasa vijana kisha
kuwafundisha dini na wao kuwainjilisha waafrika wenzao kirahisi. Kwa kusema
hivyo hatuwezi kumwacha Dr Adrian Atman katika historia ya Karema kwani ni
miongoni mwa waliokombolewa kutoka katika utumwa na kisha akawa chachu ya
kueneza injilli akiwa daktari na katekisata.
Dr
Atiman ni miongoni mwa watumwa ambaye alikuwa ni Daktari – Katekista ambaye
aliwahudumia wagonjwa na wakati huo akiwafundisha waumini neno la Mungu.
Alizaliwa huko Tundurma Maeneo ya Mto
Niger ambapo kwa sasa ni Mali, baba ake aliitwa Jucda na Mama ake Tandumosa na
walikuwa ni waislamu. Amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 66 akiwa karema, miezi
sita baada ya kufika karema Dr Atiman alimuoa Agnes Wansahira binti wa Mtemi
Mwami Mrundi ambaye Alikuwa mtemi wa Wabende mnamo mwaka 1889 na walibahatika
kupata mtoto mmoja aliyeitwa Joseph
Atiman ambaye baadae alipata upadre mwaka 1923 akiwa ni miongoni mwa mapadre wa kwanza wenyeji
Vikarieti ya Tanganyika.(Karema).
Kama
Daktari aliweza kuchanganya dawa za kizungu na za miti shamba kama sehemu ya
tiba kwa magonjwa mbalimbali. Alijitoa kwa moyo kuwahudumia wagonjwa usiku au
mchana, wakati wa baridi au joto na alipenda kusema “ napenda kubaki mwaminifu
kwa kazi yangu ya utabibu na wito wa ukatekista” . katika kazi yake ya
ukatekista alifundisha katekismu hata kwa waliofika kwaajili ya matibabu na
wanaowasindikiza, pia aliwafundisha ukatekista vijana wapatao sitini (60) huko
Kala kama njia mojawapo ya kukuza imani katika maeneo ya vikarieti ya
Tanganyika (Karema). Kwa heshima ya Dr Adrian Atmani kumejengwa zahanati
inayosimamiwa na Watawa wa MMMMA katika Parokia ya Karema (DR. ATMAN
DISPENSARY) iliyokuwa Seminari ndogo (preparatory Seminary) sasa ni chuo cha
katekesi ( BALIKUDEMBE) ambako makatekista kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo
wanapata mafunzo ya ukatekista na dini kwa ujumla.
Dr
Atiman mwaka 1894 akiwa karema aliwapokea Masista wa Kwanza wa shirikia la
Masista wa Maria Mtakatifu Malkia wa
Afrika ( White Sisters) ambao alifanya kazi nao kwa karibu katika idara ya Afya
na baada ya muda Dr Atiman Alihamishiwa Zimba moja katika Vijiji jirani kwa
Lengo la kueneza Injili na Miaka miwili baade alirudishwa karema kwa lengo la
kuanzisha seminari ndogo ya Karema. Shirika la Masista wa Maria Mtakatifu wa
Afrika lilianzishwa mnamo mwaka 1917 na Askofu Adolhe Lechaptois, kuanzishwa
kwake kulikuwa na lengo la kukuza imani hasa kuwakusanya mabinti watumwa na
kuwafundisha.
Seminari
ndogo iliyoanzishwa huko Karema ilikuwa kwa lengo la kuendelea kueneza injili
kwa kuwafundisha viongozi wa dini imani ambao hadi wanahudumu katika maeneo
mbalimbali. seminari hiyo ya karema iliwafundisha viongozi wengi akiwemo Padre
Simon Matipa aliyepata upadrisho tarehe 19.08.1960, Padre Ngua, Padre James
Sangu na Askofu wa Kwanza Mzalendo
Mwenyeji wa Karema Karolo Msakila aliyeongoza kuanzia mwaka 1958 hadi 1994 naye
alipata mafunzo katika Seminari hiyo ikiwa ni pamoja na Kadinari Polycarp Pengo na Rais wa Kenya Mwai Kibaki miaka
iliyopita
Mwaka
1967 Jimbo la Karema lilihamishwa na kuwa Jimbo la Sumbawanga ili kwenda
sambamba na mahitaji ya watu ikizingatiwa kuwa Sumbawanga ilifanywa kuwa makao makuu ya serikali na kanisa pia likaona
ni vema makao makuu ya kanisa mahalia (Jimbo) yawe hapo , hivyo Karema ikabaki
kuwa ni miongoni mwa Parokia za Jimbo la Sumbawanga.
KUSAMBAA KWA UKRISTO
MPANDA
Kutokana
na kasi ya uinjilishaji zilifunguliwa parokia mbalimbali katika maeneo ya
Mpanda na Rukwa. Katika historia hii ya Karema tuone zaidi parokia
zilizoanzishwa maeneo ya wenyeji wa |Mpanda. Ni katika harakati hizo Parokia
zifuatazo zilianzishwa, Mwaka 1903 Parokia ya Uruwila, mwaka 1904 Parokia ya
Mamba ,Milala , mwaka 1943 Inyonga , mwaka 1958 Mpanda mwaka 1964 Mwese, mwaka 1984 Katumba na
Mishamo, injili ikaendelea kuenea siku kwa siku.
Kukua
kwa imani na hitaji la kichungaji mwaka 2000 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II
aligawa Jimbo la Sumbawanga hasa parokia zilizokuwa kanda ya Mpanda na Kutangaza Jimbo jipya la Mpanda na kumteua Padre Paschal William
Kikoti kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Mpanda na tarehe 14.01.200 kuwekwa
wakfu na kuzinduliwa kwa Jimbo , na hadi sasa Karema ambapo ndio chimbuko la
Ukristo Jimbo katoliki la Mpanda imebaki kuwa Miongoni mwa Parokia za Jimbo
hilo.
MAPOKEA YA JIMBO
KATOLIKI LA MPANDA NA UKUAJI WA IMANI.
Kuzinduliwa
kwa Jimbo la Mpanda chini ya Askofu Paschal Kikoti mwaka 2000 kulipelekea
ukomavu wa imani ndani ya Mioyo ya waumini, na kipindi chote cha utume wake aliweza
kuwakusanya watu pamoja. Alihudumu kwa zaidi ya miaka 11 hadi mauti ilipomfika
mnamo tarehe 28 agosti , 2012. kutokana na jitihada zake pamoja na mapadre,
watawa na waamini injili imeendelea kuwafikia watu katika maeneo mbalimbali, na
kwa kuona hitaji hilo la uinjilishaji
alifaulu kufungua parokia zilizokuwa zimefungwa (Uruira na Milala) na
kuanzisha nyingine mpya (Ilembo na Shanwe), pia kuanzisha seminari ndogo ya
jimbo ( Mt.Yohane Paulo II- Mpandandogo) ikiwa ni jitihada za kuwapatia elimu
stahiki na malezi vijana na maandalizi ya kuwa mapadre wa kulihudumia kanisa.
Sambamba
na hilo suala la elimu na afya hakuliacha mbali kwani alianzisha shule ya
sekondari ya Mt Maria Mpanda ili watoto wa wenyeji wa Mpanda na maeneo mengine
ya nchi wapate malezi na elimu hapo, na alifanikiwa kuanzisha zahanati kadhaa
na vituo vya afya kwa lengo lilelile la wamisionari kumkomboa mwanadamu kiroho
na kimwili. Hadi sasa Jimbo katoliki la Mpanda lina Jumla ya Parokia 16 ambazo
ni Mpanda, Karema , Inyonga , Uruwila, Milala, Shanwe, Mishamo, Ilembo, Mamba, Usevya,
Katumba, Kanoge, Buhingu , Utinta, Mwese na Mpanda ndogo.
Wapo
Madre wapatao 25 wanaohudumu Jimboni hapo wakiwemo wageni kutoka nje ya Jimbo
na wenyeji wao. Jimbo katoliki la Mpanda linaongozwa na Mhashamu Baba Askofu
Gervas J. Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Katika kukuza imani, shirika la Wabenediktini wameanzisha kituo cha malezi ya
utawa (masista) katika parokia ya Uruira na hivi kuwalea mabinti wenye wito wa
utawa na hatimaye wafanye kazi za kitume katika kanisa.
Harakati
za kueneza injili zilienda sambamba na Kuwakomboa watumwa kutoka katika mikono
ya wakoloni, Kuanzisha shule, kuanzishwa kwa Mashiriki ya kitawa , Kuanzishwa
kwa Seminari na Kujenga vituo vya Afya na sasa ukristo Jimbo la Mpanda unakuwa
kwa kasi ya hali ya juu.
CHANGAMOTO ZA KUENEA
KWA DINI
o
Hali ya hewa, hii inatokana na
kubadilika kwa mazingira, hususani kwa mapadre wamisionari waliokutana na hali
tofauti ya hewa iliyoambatana na magonjwa ya milipuko na mwingiliano wa wageni.
o
Migogoro ya hapa na pale kati ya watemi
na wamisionari katika harakati za kubadili itikadi ya tamaduni zao.
o
Kuwatoa watu kwenye mtazamo wa upagani
hadi kumjua Mungu ni jambo ambalo katika kipindi hicho haikuwa rahisi. ( mind
of colonization) ilichukua muda kuamini kuwa wamisionari walikuja kwa ajili ya
ukombozi
Wakati
Kanisa Katoliki Linaadhimisha Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara tangu
kuingia kwake kutoka Zanzibar mwaka 1868, Jimbo katoliki la Mpanda litakuwa pia
linatimiza miaka 133 ya ukristo tangu ulipoingia Karema Mwaka 1885 kutokea
Bagamoyo.
Kwa Mawasiliano Zaidi
Piga Simu namba 0757 058 068
TUMSIFU
YESU KRISTO.,,,,,,,,,,,,,,,,…………………………………
Amen! Mungu yu pamoja nanyi katika kazi ya Utume. "Moyo Mkuu"
ReplyDelete