Tuesday, April 16, 2019

MAPADRE: TUISHI UKUHANI WETU



MAPADRE: TUISHI UKUHANI WETU…………………………….   11/04/2019

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu teule la Mbeya Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga amewataka Mapadre wa kanisa katoliki kote nchini kuuishi Upadre wao.

Mhashamu Baba Askofu ameyasema hayo wakati wa Misa Takatifu ya Krisma ( Misa ya Kubariki Mafuta) iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kanisa kuu Jimbo Katoliki Mpanda alhamisi ya tarehe 11 ambapo Mapadre, Watawa wa Kike na wakiume, vyama mbalimbali vya kitume kutoka Parokia 16 za Jimbo la Mpanda walihudhuria  .

Amesema kuwa Siku hii kwa upande wa Mapadre ni siku ya kukumbuka ukuhani wao, kujitathimini juu ya daraja takatifu la Upadre, kutambua kuwa uwepo wao katika kanisa ni faraja kwa waliokata tamaa, kutangaza habari njema, kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika misingi ya imani ya Kanisa Katoliki.

“ kila Padre afanye tathimini ya Ukuhani wake, je? unafanana na Yesu kwa kiasi gani? Yesu ambaye ni kielelezo cha Amani, Utii, Upendo, ambaye aliyatoa maisha yake hata kufa  msalabani kwa ajili ya dhambi zetu wanadamu, Mnyenyekevu na mwenye upendo?. Waumini washuhudie huduma za mapadre na wajisikie kufanyika wana wa Mungu”.

Baba Askofu ameelezea kuwa Misa ya Kubariki mafuta hufanyika kila mwaka ambapo mafuta hubarikiwa ili kuweza kutoa huduma mbalimbali kwa waumini na ameongeza kuwa kwa kupakwa mafuta haya tutapata utakaso na kuwa wapya mbele ya mwenyezi Mungu kwa kuwa ni nguvu ya uovu.

Pamoja na hayo amewakumbusha waumini kufanya toba ya ndani  kipindi hiki cha kwaresma ambacho kinaelekea mwisho ili Yesu anapofufuka afufuke na kondoo wake, Kuishi maisha ya upendo, utii na unyenyekevu huku kila mmoja akitafakari matendo makuu ya mwenyezi Mungu katika Maisha yake.

“tunaelekea mwisho wa kipindi cha Kwaresma, kipindi cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, sasa tujiandae kufufuka pamoja naye, tutafute kufanya toba ili tuwe huru mbele yake kwani giza likizidi sana jua Mwanga unakaribia” nawatakia Maandalizi Mema ya Sikukuu ya Pasaka. Amesema Gervas Nyaisonga

Na Suzan Kanenka
Mkurugenzi wa Mawasiliano
Jimbo Katoliki Mpanda

No comments:

Post a Comment