Tuesday, April 16, 2019

MAPADRE: TUISHI UKUHANI WETU



MAPADRE: TUISHI UKUHANI WETU…………………………….   11/04/2019

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu teule la Mbeya Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga amewataka Mapadre wa kanisa katoliki kote nchini kuuishi Upadre wao.

Mhashamu Baba Askofu ameyasema hayo wakati wa Misa Takatifu ya Krisma ( Misa ya Kubariki Mafuta) iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kanisa kuu Jimbo Katoliki Mpanda alhamisi ya tarehe 11 ambapo Mapadre, Watawa wa Kike na wakiume, vyama mbalimbali vya kitume kutoka Parokia 16 za Jimbo la Mpanda walihudhuria  .

Amesema kuwa Siku hii kwa upande wa Mapadre ni siku ya kukumbuka ukuhani wao, kujitathimini juu ya daraja takatifu la Upadre, kutambua kuwa uwepo wao katika kanisa ni faraja kwa waliokata tamaa, kutangaza habari njema, kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika misingi ya imani ya Kanisa Katoliki.

“ kila Padre afanye tathimini ya Ukuhani wake, je? unafanana na Yesu kwa kiasi gani? Yesu ambaye ni kielelezo cha Amani, Utii, Upendo, ambaye aliyatoa maisha yake hata kufa  msalabani kwa ajili ya dhambi zetu wanadamu, Mnyenyekevu na mwenye upendo?. Waumini washuhudie huduma za mapadre na wajisikie kufanyika wana wa Mungu”.

Baba Askofu ameelezea kuwa Misa ya Kubariki mafuta hufanyika kila mwaka ambapo mafuta hubarikiwa ili kuweza kutoa huduma mbalimbali kwa waumini na ameongeza kuwa kwa kupakwa mafuta haya tutapata utakaso na kuwa wapya mbele ya mwenyezi Mungu kwa kuwa ni nguvu ya uovu.

Pamoja na hayo amewakumbusha waumini kufanya toba ya ndani  kipindi hiki cha kwaresma ambacho kinaelekea mwisho ili Yesu anapofufuka afufuke na kondoo wake, Kuishi maisha ya upendo, utii na unyenyekevu huku kila mmoja akitafakari matendo makuu ya mwenyezi Mungu katika Maisha yake.

“tunaelekea mwisho wa kipindi cha Kwaresma, kipindi cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, sasa tujiandae kufufuka pamoja naye, tutafute kufanya toba ili tuwe huru mbele yake kwani giza likizidi sana jua Mwanga unakaribia” nawatakia Maandalizi Mema ya Sikukuu ya Pasaka. Amesema Gervas Nyaisonga

Na Suzan Kanenka
Mkurugenzi wa Mawasiliano
Jimbo Katoliki Mpanda

Monday, April 15, 2019

Vijana msiwe kama Nyama ya Jokofu



VIJANA MSIWE KAMA NYAMA YA KWENYE JOKOFU ……………11/04/2019

“ Vijana legelege, wasiopenda kufanya kazi, wanaotegemea kutunzwa na wazazi wao muda huo umekwisha, fanyeni kazi kwa bidii ili muweze kutoka hapo mliposimama miaka yote”

Maneno hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu teule la Mbeya Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga katika kongamano la vijana Jimboni Mpanda.

Kongamano hilo lililofanyika Parokia ya Kanisa Kuu Mpanda katika ukumbi wa Mikutano kuanzia tarehe 10-14.4.2019 lilifunguliwa rasmi na Mhashamu Baba Askofu sambamba na Mkurugenzi wa Vijana Jimbo Padre JohnBosco Misigalo ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mamba liliwakutanisha vijana zaidi ya 200 kutoka Parokia 14 kati 16 za Jimbo.

Wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo Mhashamu Baba Askofu alikumbushia majukumu ya vijana katika kanisa ambapo amesema kuwa “ Uzima wa Kanisa ni Vijana”, vijana hai hulijenga kanisa kwa majitoleo mbalimbali lakini kulijenga kanisa inategemeana na namna ambavyo vijana mnashiriki katika shughuli kwa ushirikiano, umoja , unyenyekevu na mahusiano mazuri. Haya yote hayawezi kufanikiwa ikiwa kijana atakuwa ametengeneza mazingira mabovu ya kujitegemea kama “NYAMA YA JOKOFU”.

Nyaisonga amesema ulimwengu wa sasa umejawa na vijana wengi wenye taaluma mbalimbali, wasomi, wajasiliamali na makundi mengine, “Tumieni ujuzi mliopewa na mwenyezi Mungu kwa kufanya kazi kwa bidii, kwa kufanya hivo mtazikomboa familia zenu na kanisa la Mungu. Amesema kama mwaka uliopita ulikwama mahali basi angalia namna ya kupiga hatua ndefu zaidi kufikia malengo, lakini katika yote mkumbuke kusali, kufanya toba ili maisha yenu yawe yanayompendeza Mungu siku zote.

Aidha amewapongeza vijana wote kwa moyo wa majitoleo kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo pasi na changamoto zinawakabiri” nimefurahi sana kuwaona kwa wingi, sasa naamini Jimbo la Mpanda lina hazina kubwa hapo baadae, muendelee kuwa na moyo huo na siku zote mpende kushiriki kazi za kanisa kwani maisha ya hapa duniani ni ubatili Mtupu.

Mwisho : Mhashamu Baba askofu amewapongea kwa namna ya pekee vijana wakatoliki kote nchini wanaotumia vipawa walivyojaliwa na mwenyezi Mungu kufanya kazi za Kanisa bila kujali muda wanaopoteza na nguvu nyingi, “ lakini katika yote niwatie moyo yeyote afanyaye kazi kwa bidii hupata ujira wake, kwa kufanya kazi za kanisa mnajiwekea hazina isiyofutika mbinguni.
Nawatakia maandalizi mema ya Sikuku ya Pasaka , tukumbuke kufanya toba ili tufufuke pamoja na Yesu Mkombozi wa Miasha Yetu.


NA SUZAN KANENKA
MKURUGENZI WA HABARI
JIMBO KATOLIKI MPANDA