Sunday, March 24, 2019

WAUMINI WAPOKEE MABADILIKO





WAAMINI WAPOKEE MABADILIKO YA UONGOZI KAMA CHACHU YA MAENDELEO

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu Mkuu wa Jimbo kuu Teule la Mbeya na Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga amewataka waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Inyonga kupokea mabadiliko ya Uongozi  kama ishara ya kupanua undugu na Kukuza Maendeleo.

Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu Parokiani Inyonga,  wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya Kichungaji na kupata wasaa wa kuagwa na waumini wa Parokia kutokana na uteuzi aliopata wa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya mwishoni mwa mwezi wa 12, 2018.

Baba Askofu amesema “yatupasa kupokea mabadiliko mda wowote wa viongozi, kwa kuwa kanisa katoliki lina taratibu zake za hasa katika kuteua viongozi mbalimbali, kuteuliwa kwangu kuwe ni njia mojawapo ya kuongeza undugu baina yetu, najua waumini wengi walipokea taarifa hizi kwa mshtuko kidogo lakini niwatie moyo na jueni tuko pamoja katika uchungaji”

Ameongeza kuwa yatupasa kuwaombea viongozi wa kanisa ili waendelee kuifanya kazi ya kuchunga kondoo waliokabidhiwa, ushirikiano, upendo, uwe nguzo miongoni katika kutekeleza majukumu ya Kikanisa.  Amewasihi pia Makatekista kumsadia Paroko  kufundisha dini.

Licha ya yote amewataka wakristo kufanya toba ya ndani katika kipindi hiki cha Kwaresma ili kuwa karibu na Mungu, kujitoa kwa bidii kufanya kazi kanisa, kuwasaidia wahitaji mbalimbali waishio katika hali ngumu kiuchumi.

Misa Hiyo Takatifu ilihudhuliwa na baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mh Rachel Steven Kasanda ambaye pia alipata nafasi ya kusema yafuatao. “ Nipende kumshukuru Mungu kwa Kuwa na kiongozi ambaye anajua mahitaji ya waumini wake, nakuombea maisha marefu yenye amani hata uko uendeako tunaamini tuko pamoja, Mungu akujaalie Afya ya Roho na Mwili uendelee kulichunga kanisa na kondoo uliokabidhiwa. Pamoja na yote ninakutakia safari njema uendekao…

Mh Baba Askofu pia amewataka wazazi na walezi kuwapatia elimu watoto wao, “ wapelekeni watoto wenu shule wapate elimu na hatimae waje kuwa nguzo imara katika kulijenga taifa la Mungu na kujikomboa kutoka katika hali duni ya uchumi, msiwaozeshe watoto wangali wadogo, msiponze na ngombe wa vijisenti  vinavyopelekea mtoto kukosa haki zake za msingi, watoto ni sharti wapate elimu.

Mh Baba Askofu pamoja na mambo mengine amefungua rasmi Sala ya Jubilei ya Miaka 75 ya Ukristo Parokia ya Inyonga ambayo itaanza kutumika kwa ajili ya kuendelea kuiombea Parokia ya Inyonga hadi kilele cha maadhimisho ya Jubilei hiyo zinazotarajia kufanyika mapema mwezi wa nane mwaka huu.


Mwisho, ninawatakia Amani na Furaha siku zote , nasisitiza Upendo na Mshikamano miongoni mwetu, tusaidiane , tushauriane ili tuweze kufikia malengo tunayokusudia. Lakini kubwa zaidi tuwafundishe waamini wetu kuishi maisha ya utakatifu wangali duniani kwa njia ya kufanya toba.

TUMSIFU YESU KRISTO

NA Suzan Kanenka
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano
Jimbo Katoliki la Mpanda                                                                                   

No comments:

Post a Comment